Muimbaji wa Nigeria, Simi, amelazimika kutoa ufafanuzi baada ya tweets zake za zamani, zilizoandikwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, kuibuliwa tena na kuzua mjadala mkali mitandaoni.
Tweets hizo za mwaka 2012 na 2013 zimetafsiriwa vibaya na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii, huku wengine wakizichukulia kama zisizofaa.
Mjadala huo umeibuka siku chache baada ya Simi kutoa kauli tata kuhusu suala la ubakaji na wanaume wengi kuhusika katika vitendo hivyo, jambo lililosababisha baadhi ya watu kuchunguza historia yake ya mitandao ya kijamii.
Katika tweet nyingine ya mwaka 2013, aliandika kuwa anapenda kuwabusu watoto wa daycare kwa sababu ni “wazuri sana,” na kuongeza kuwa “I am crazy about them.”
Baadhi ya wakosoaji walitafsiri maneno hayo kama yasiyofaa na kumshutumu kwa kuwa na mawazo yasiyostahili kuhusu watoto.
Februari 23,Simi ametoa maelezo ya kina akisema kuwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 23 na alikuwa akiishi kwa mama yake. Amesema alikuwa akitweet mambo ya kila siku, ikiwemo matukio ya kuchekesha yanayohusisha watoto katika daycare hiyo.
Simi amesisitiza kuwa hajawahi kuwa mtu mwenye tabia mbaya na kwamba maneno yake yanapotoshwa ili kuendana na simulizi zisizo za kweli.
Amekiri kuwa timu yake imefuta baadhi ya tweets kutokana na unyeti wa suala hilo kwa familia yake, ingawa hakutaka zifutwe mwanzoni.
Aidha, amesisitiza msimamo wake wa kupinga ubakaji na unyanyasaji wa kingono, akisema: “Nimekuwa nikiongea dhidi ya ubakaji hata kabla hamjanijua. Sio vazi nililovaa, ni mimi halisi. Nilisema acheni kuwabaka wanawake. Ninasimama kwenye hilo.”
