
Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha sita huku ufaulu wa jumla ukiwa asilimia 99.95 kwa watahiniwa 126,135 waliofanya mtihani, sawa na ongezeko la asilimia 0.03 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2024 ambao ulikuwa asilimia 99.92.
Akitangaza matokeo hayo Julai 7, 2025 katika ofisi za Necta Zanzibar, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Profesa Said Mohamed, amesema watahiniwa 790 hawakufanya mithani sawa na silimia 0.62.
Amesema ufaulu wa watahiniwa kwa kuzingatia jinsi unaonesha kuwa wasichana waliofaulu ni 61,953 sawa na asilimia 99.95, huku wavulana wakiwa 63, 826 sawa na asilimia 99.95.
Amesema takwimu zinaonyesha jumla ya watahiniwa 125, 375 sawa na asilimia 99.62 wamepata ufaulu wa madaraja ya kwanza hadi la tatu, kati ya hao waliopata daraja la kwanza ni watahiniwa 61, 120 sawa na asilimia 48.57, daraja la pili ni 49, 385 sawa na asilimia 39.24.
Hata hivyo Baraza la Mitihani la Tanzania limefuta matokeo ya watahiniwa 71, wakiwemo 70 wa mtihani wa kidato cha sita na mmoja wa ualimu daraja A (GATCE).
Profesa Said Mohamed amesema matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2) (i) na (j) cha shera ya baraza la mtihani sura ya 107.
Kwa mujibu wa Profesa Mohamed amesema baadhi yao waliingia na simu, saa janja kwenye vyumba vya mtihani na kusaidiana kwenye mtihani.