
Katika pilikapilika za soko kuu Kajetia alimaarufu kama “Dubai,” lililopo katikati ya jiji la kibiashara Kumasi, Ghana, kuna ukweli mgumu uliojificha nyuma ya mizigo inayobebwa. Huu si ukweli wa biashara, bali ni wa maisha ya wanawake na wasichana wadogo, wanaojulikana kama “Kayaye”.
Neno “Kayayei” linalotumiwa kuelezea wapagazi wanawake nchini Ghana si la asili kwa lugha ya Twi nchini Ghana, kama wengi wanavyodhani. Neno hili linaunganisha maneno mawili kutoka lugha tofauti: “Kaya” (mzigo) kutoka Hausa, na “Yei” (wanawake) kutoka Ga. Hivyo, “Kayayei” linamaanisha moja kwa moja “wanawake wabeba mizigo”, huku umoja wake ukiwa ni “Kayayoo”.
Cha kushangaza zaidi kwenye soko hili ni kuwa wanaume wabeba mizigo si wengi kama tudhanivyo. Badala yake, idadi kubwa ya kazi hii ngumu inafanywa na wanawake vijana, wengi wao wakitoka mikoa ya kaskazini mwa Ghana na hata nchi jirani.
Wabeba mizigo hawa huanza kazi mapema mno, saa kumi asubuhi, na kufikia saa nne asubuhi, miili yao inakuwa imechoka kabisa kutokana na ugumu wa kazi yenyewe. Maisha yao yamejaa changamoto, ikiwemo ukosefu wa malazi ya uhakika baada ya siku ndefu ya kazi. Ni hali ya maisha magumu na ukosefu wa fursa za kielimu au ajira zinazowasukuma kwenye kazi kama hii.
Hata hivyo, kuna mwanga wa matumaini kwa wasichana hawa. Shirika lisilo la kibiashara la SAFE-CHILD ADVOCACY (SCA), lenye makao yake makuu Kumasi,linaloendeshwa na kusimamiwa na Jimbo Kuu Katoliki la Kumasi Kupitia Masista wa shirika la “Mabinti wa Upendo” chini ya usimamizi wa Sr. Olivia Umoh limejitolea kuwasaidia.
Shirika hili la kitawa kwenye Kanisa Katoliki lilianzishwa na Mtakatifu Vincent de Paul na Mtakatifu Louise de Marillac. Kazi yao kuu ni kutoa huduma kwa maskini, wagonjwa na wale wanaohitaji msaada na haswa kuwafikia wale waliosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Kwa hapa nchini Ghana, SCA linawapatia wanawake na watoto hawa msaada wa kisheria na kuwawezesha kupata elimu ya msingi, sekondari na ufundi likijaribu kuwaondoa kwenye mzunguko huu wa maisha magumu na kuwapa nafasi ya kujenga mustakabali bora wa maisha.
Mpango wa “Elimu Mtaani” ni sehemu moja tu ya kazi nyingi ya shirika la SAFE-CHILD ADVOCACY (SCA). Mpango huu unawalenga wasichana wanaofanya kazi ya kubeba mizigo, almaarufu kama “Kayayei”, kwa kuwapa masomo muhimu yanayohusu ustawi wao.
Mafunzo hayo yanachukua saa moja au mbili ambapo wasichana hawa hupewa elimu ya kiroho, kimaadili, na msaada wa kisaikolojia. Lengo kuu ni kuwajengea uwezo na kuwapa matumaini licha ya ugumu wa maisha.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayokabili mpango huu ni uchovu wa wasichana hao. Kazi yao huanza mapema saa kumi asubuhi, na kufikia saa nne asubuhi, wengi wao tayari wanakuwa wamechoka sana, jambo ambalo hufanya iwe vigumu kwao kunufaika kikamilifu na mafunzo hayo.
Kwa muda wa miaka 20 sasa, Mabinti wa Upendo kwa kushirikiana na Safe-Child Advocacy (SCA) wamekuwa kitovu cha matumaini, kwa kuwapatia“Kayayei” hifadhi na nuru mpya ya maisha. Licha ya nuru hii mpya, shirika hilo limepanua wigo wake kwa kuanzisha vituo vitatu muhimu jijini Kumasi, Ghana. Mosi ikiwa ni Kituo cha Kupumzikia alimaarufu kama (Drop-in-Centre). Kituo hiki kimeanzishwa kama mahali salama ambapo wasichana hawa wanaweza kupumzika au kupiga gumzo bila hofu yoyote.
Wanaruhusiwa kucheza michezo mbalimbali na kupata muda wa kupumzisha akili na miili yao kutokana na kazi ngumu wanayoifanya. Pili ni Kituo cha Mafunzo ya Ufundi cha Mtakatifu Louise (St. Louise Vocation Training). Kituo hiki kinatoa hifadhi kwa wasichana walio katika hatari, ambao nyumbani kwao si salama. Wengi wao wamekimbia manyanyaso, unyanyasaji wa kingono, au ndoa za kulazimishwa. Kituo hiki kinawapa mafunzo ya ufundi, hifadhi ya muda mfupi na ya muda mrefu, huku wengine wakiokolewa kutoka mikononi mwa biashara haramu ya binadamu na kurudishwa kwa jamaa zao.
Tatu ni Kituo cha Kulea Watoto cha Mtakatifu Vincent de Paul (St. Vincent de Paul Day Care Centre) Kituo hiki kinawalenga kina mama wanaofanya kazi sokoni na mitaani katika mazingira magumu. Wanawapeleka watoto wao hapa ili wawe salama wakati wao wakienda kutafuta riziki. Kituo hiki kinawasaidia kina mama hawa kuepuka hatari za kuwabeba watoto wao wanapofanya kazi ngumu.
Unaweza kubadilisha maisha ya wanawake na watoto wao kwa kutoa msaada, elimu, na fursa za kiuchumi popote pale ulipo. Anza kwa kushirikiana na mashirika yanayojitolea kuwasaidia, kisha waelimishe jamii kuhusu changamoto wanazopitia.
Hatua hii ndogo inaweza kuwapa tumaini jipya na kuwahakikishia mustakabali mwema wa maisha. Okoa maisha ya mwanamke kwa kumtua mzigo mgumu wa maisha kichwani popote ulipo haswa wanawake na watoto waliosukimizwa pembezoni mwa jamii.