Samwel Masunzu- Kibondo, KIGOMA
Uongozi wa kijiji cha Kitahana kata ya Kitahana wilayani Kibondo mkoani Kigoma wametoa cheti na zawadi kwa Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Muyaga kwa kuendelea kusimamia taaluma na ufaulu mzuri kwa wanafunzi.
Cheti na zawadi hiyo vimekabidhiwa na Katibu wa Mbunge Jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo kwa niaba ya uongozi wa kijiji hicho katika halfla ya kukabidhi madawati 42 kwa shule za msingi Muyaga, Kahama na Kasebuzi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kitahana Bw. Eriabi Kabuga, pamoja na viongozi wa kata, Afisa Mtendaji Bw. Fundi Hamis na diwani wa kata hiyo Bw. David Rafaeli wamesema uamzi huo ni kutokana na jitihada za mwalimu huyo za kusimamia taaluma na kuendelea kuongoza katika ufaulu ngazi ya kata na kuwa katika shule 10 bora kiwilaya na malengo ni kushika nafasi nzuri ngazi ya mkoa na Taifa.
Akizungumza na Radio Kwizera Mwalimu Majaliwa Erasto amesema kuendelea kuimarika kwa taaluma ni kutokana na ushiriki mzuri wa serikali ya kijiji, Uongozi wa shule na wazazi hasa katika kutoa huduma ya chakula shuleni na wanafunziΒ 3 kwa matokeo ya mwaka 2025 walichaguliwa kati ya wanafunzi wenye vipaji maalumu kwa matokeo ya darasa la saba.
