
Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza rasmi kwamba Uwanja wa Maonyesho ya Wakulima (Nanenane) uliopo jijini Dodoma sasa utaitwa Dkt. John Malecela, mmoja wa viongozi waandamizi waliolitumikia taifa kwa muda mrefu.
Akizungumza leo katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane kitaifa, Rais Samia amesema uamuzi huo umetokana na mchango mkubwa alioutoa Dk Malecela kwa Taifa, hususan kwenye sekta ya kilimo na uongozi kwa ujumla.
Uamuzi huo wa kuupa jina la uwanja ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango wa wazee wa taifa ambao bado wanaendelea kushiriki katika maendeleo ya nchi, licha ya kustaafu kwao kiserikali.
Katika hatua nyingine Rais Samia ametoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha kuwa Viwanja vya John Malecela vilivyopo Nzuguni, jijini Dodoma, vinakuwa makao makuu ya huduma za ugani nchini.
Amesema kutokana na kuwepo kwa maduka ya pembejeo za kilimo, bidhaa za mifugo na uvuvi katika viwanja hivyo, na kwa kuwa eneo hilo litaendelea kufanya kazi mwaka mzima, ni vyema huduma za ugani zikahamishiwa hapo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma zote ndani ya eneo moja.
Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa wakati viwanja hivyo vikianza kuwa makao makuu ya huduma za ugani, maeneo mengine nchini yaendelee kutoa huduma hizo ili kuhakikisha wakulima wote wanafikiwa.