
Vijana 12,261 kutoka mikoa ya Geita, Kagera, Tabora na Tanga wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kuwawezesha kiuchumi unaotekelezwa katika maeneo yaliyopitiwa na Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) katika awamu ya kwanza.
Mradi huo ni sehemu ya mpango wa uwajibikaji wa kampuni hiyo kwa jamii wakati na baada ya ujenzi wa bomba hilo.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo uliofanyika jana katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko amesema mradi wa bomba la mafuta utasaidia vijana kukabiliana na changamoto za ajira na kipato zinazowakabili.
Amesema hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kukamilika Julai 2026 huku Serikali ya Tanzania ikiwa tayari imetoa Shilingi trilioni 1.125
Dkt. Biteko amesema kupitia mradi huo, kampuni 200 za Kitanzania zimeajiriwa na fedha zinazopatikana zinazunguka kwenye maisha ya kawaida ya Watanzania hasa wale wanaojishughulisha na kazi za kawaida.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Patrobas Katambi amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametengeneza mipango mikakati ya kuhakikisha vijana wanapewa fursa za ajira na mitaji kwenye maeneo mbalimbali, ambapo mpango wa YEE ni kielelezo cha matokeo ya mipango hiyo.
Mkuu wa Mkoa Geita, Martine Shigella akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa inayopitiwa na mradi wa EACOP amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo wananchi wa Geita wamenufaika nayo kwa namna mbalimbali.