
Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera Dkt. Abel Nyamahanga amewataka viongozi wa Vijiji na Kata kusimamia kikamilifu uuzaji wa kahawa mbichi kwa wakulima ili kuweza kuvuna zenye ubora unaotakiwa na kuongeza ubora wa thamani wa zao hilo.
Dkt. Nyamahanga amesema hayo wakati wa kikao cha wadau wa kahawa kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na kubainisha kuwa kahawa zote zitakuwa zinauzwa kwa njia ya mnada kwenye vyama vya msingi pekee.
Amesema kuwa jukumu la kusimamia utoroshaji wa zao hilo sio la Serikali pekee bali ni la kila mdau hivyo endapo mtu akibainika anafanya kitendo hicho atachukuliwa hatua za kisheria.
Afisa kilimo Wilaya ya Muleba Bw. Daudi Kingu, amesema kwa msimu wa mwaka huu Wilaya hiyo inatarajia kuvuna tani 5,816 za kahawa ya maganda na itapata ushuru wa zaidi ya shilingi milioni 800 ingawa bado kuna changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi na utoroshaji wa zao hilo kwenda nje ya nchi.