
Wasanii na wadau wa muziki wa Jamaica wanaiomba tena Recording Academy kuanzisha vipengele viwili tofauti vya Grammy: Best Reggae Album na Best Dancehall Album.
Kwa mujibu wa wasanii na wadau Wanasema muziki wa Reggae na Dancehall umeendelea kubadilika kwa sauti, mashabiki na matokeo yake duniani, hivyo unastahili utambulisho tofauti.
Kwa sasa, Academy inajumuisha muziki wote wa Jamaica kwenye kipengele cha Best Reggae Album, jambo ambalo wakosoaji wanasema halitendei haki Dancehall yenye sauti kali, mashairi ya ujasiri na ushawishi mkubwa kimataifa.
Mwezi Novemba 2022, Mkurugenzi Mkuu wa Recording Academy, Harvey Mason Jr., alikiri mjadala huo na kusema kuwa kutenga vipengele hivyo kunawezekana.
Hata hivyo, kauli yake ilipingana na ile ya mtayarishaji na meneja wa muziki Cristy Barber, aliyewahi kuteuliwa Grammy, ambaye Machi 2022 alisema ni vigumu Dancehall kupata kipengele chake kutokana na wafanyakazi wachache na mwelekeo wa Academy kupunguza vipengele badala ya kuongeza.
Barber alionya pia kuwa badala ya kushinikiza tuzo mpya, wasanii wanapaswa kulinda uhalisia wa kipengele cha sasa cha Best Reggae Album, akihofia huenda siku moja kikaondolewa au kupoteza thamani yake.