
Baadhi ya wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga katika kituo kikuu cha mabasi ya abiria mkoa wa Geita wameishukuru serikali kutoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya cha mabasi mkoani humo.
Wakizungumza na redio kwizera kwa nyakati tofauti Prosper Vitus, Elias Maneno na Boniphase Madundo wamesema kutekelezeka kwa mradi huo kutawasaidia kutokana na adha ya kuzama nyakati za masika.
Wamesema kituo cha mabasi wanachotumia kwa sasa wakati mwingine hujaa maji nyakati za mvua jambo ambalo huathiri mzunguko wa biashara zao na kwamba hawana budi kuipongeza serikali kwa kuanza kutatua changamoto hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba amesema fedha za mradi wa ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya mkopo wa benki ya dunia wenye lengo la kutekeleza mradi wa uboreshaji miundombinu ya miji Tanzania (TACTIC).