Wakili wa kujitegemea, Peter Madeleka, ametoa wito wa kufanyiwa marekebisho kikatiba ya namna ya kuwapata majaji, akidai kuwa sifa za sasa za upatikanaji wa majaji ni “nyepesi mno” na zimepitwa na wakati kulinganisha na vigezo vya kimataifa.
Akizungumza leo, Januari 14, 2026, Madeleka amesema mfumo wa sasa wa kumpata Jaji kupitia uteuzi wa Rais bila ushindani wa wazi, unadhoofisha uhuru wa mahakama na kuleta mashaka ya migongano ya kimaslahi
Amelinganisha hali hiyo na nchi jirani ya Kenya, ambapo mchakato wa kuwapata majaji unahusisha kutangazwa kwa kazi, usaili wa wazi, na ushindani kulingana na rekodi ya uadilifu na uzoefu.
Wakili huyo amebainisha kuwa mfumo wa uteuzi unamfanya Jaji kuwa na “deni la fadhila” kwa mamlaka iliyomteua. Ameeleza kuwa ikiwa Jaji anajua kupanda kwake cheo kwenda Mahakama ya Rufani kunategemea mkono wa Rais, ni vigumu kwake kutoa maamuzi dhidi ya Serikali hata kama sheria iko wazi.
Kama suluhisho, Madeleka amependekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa wazi ambapo kazi za ujaji zinatangazwa na usaili wa hadhara kufanyika. Amependekeza pia wananchi wapewe nafasi ya kuwasilisha taarifa za uadilifu wa waombaji kabla ya kuteuliwa, ili kumpata kiongozi mwenye kibali cha umma na taaluma.