Michael Mpunije- Kasulu, KIGOMA
Mashirika ya World Vision Tanzania na Good Neighbors Tanzania yanayotekeleza mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI) yamekabidhi mashine na vifaa 48 kwa washindi wa andiko bora la kilimo biashara kutoka wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko mkoani Kigoma.
Mashirika hayo yanayotekeleza mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini kupitia shirika la mpango wa chakula duniani WFP ambapo vifaa hivyo vitasaidia wakulima kulima kwa tija na kuongeza kipato.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano Mwakilishi wa Meneja wa Kanda kutoka shirika la World Vision Tanzania Eric Kidohela amesema mradi huo unalenga kuendeleza mawazo ya wakulima kutoka kilimo cha cha mazoea hadi kilimo chenye tija.
Meneja wa Mradi Kutoka shirika la WFP Kasulu, Bw. Heshima ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia mashirika ya World vision na Goodneighbors katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima wadogo wadogo Mkoani Kigoma.
Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi viwanda na Uzalishaji Mkoa wa Kigoma James Peter amesisitiza kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuendeleza kilimo na kuongeza uzalishaji kupitia sekta ya Kilimo Katika mkoa wa Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, amewashauri wakulima kuthamini na kutunza vifaa hivyo.

Baadhi ya wakulima ambao wamepatiwa vifaa, wamesema vitarahisishia shughuli za kilimo na kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili hapo awali.
Miongoni mwa vifaa ambavyo vimetolewa kwa vikundi na watu binafsi ni Pamoja na power tiller 1, mashine 3 za umwagiliaji, mashine 21 za kupandia na kuwekea mbolea, 2 za kupalilia, 2 za kushonea magunia, 2 za kupukuchua mahindi, mipira 3 kwa ajili ya umwagiliaji, mashine 4 za kusukuma maji Pamoja na mashine 2 za kupulizia viatirifu, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50.

