
Mkuu wa wilaya ya Ngara mkoani Kagera Kanali Mathias Kahabi amewataka wakuu wa idara wote wilayani humo kuwa waaminifu katika kusimamia miradi yote ya maendeleo.
Ametoa rai hiyo leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi ya maji wilayani humo ambapo amesema endapo miradi haitasimamiwa na kutekelezwa kwa uaminifu itapelekea miradi hiyo kutekelezwa chini ya viwango.
Kanali Kahabi ameongeza kuwa licha baadhi ya watendaji katika wilaya ya Ngara kufanya kazi nzuri bado wamekuwa wakikwamishwa na wakandarasi wasiokuwa waaminifu katika kutekeleza miradi ya maendeleo
Naye mkurugenzi wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira wilaya ya Ngara Mhandisi Jumanne Magungu amesema kuwa mamlaka hiyo inatarajia kuongeza mtandao wa maji ili kuhakikisha huduma hiyo inakuwa ya uhakika kwa wakazi wa Ngara
Mpaka sasa serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji wilayani Ngara na jumla ya visima vinne mpaka sasa ndio vyanzo vikuu vya kusambaza huduma hiyo.