
Na, Amos John
KISHAPU
Wananchi wa kijiji cha Ilindilo kata ya Itilima halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wameiomba halmashauri ya wilaya hiyo kusaidia kumalizia ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi waliouanza kwa nguvu zao.
Wito huu umetolewa na Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Mwamala Bw. Lukasi Masingija wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya Shule hiyo wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa madawati 80 yaliyotolewa wadau wa maendeleo.
Mwalimu Masingija ameeleza kuwa kufuatia changamoto hiyo wanafunzi wa darasa la kwanza na la pilli wanalazimika kusomea chini ya mti kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo.
Akitoa ufafanuzi Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya hiyo, David Mashauri amekiri uwepo wa changamoto hiyo na kueleza kuwa halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya kukabilisha maboma hayo ambayo ni sehemu ya maboma 78 yanayo takiwa kukamilishwa ujenzi wake katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.