
Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria, Zacharia Obad, ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kupokea rushwa, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Mwanza, Obad amesema inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wa kisiasa wakitumia fedha kuwashawishi wananchi kuhudhuria mikutano au kutaka uungwaji mkono
Ameongeza kuwa demokrasia ya kweli haiwezi kujengwa kwa misingi ya ushawishi wa kifedha bali kwa sera, maadili na uwajibikaji wa kweli kutoka kwa viongozi wanaowania nafasi za uongozi na kuwataka wananchi kuwapima wagombea kwa hoja na si kwa zawadi au fedha.
Aidha Bw. Obad amesisitiza kuwa CHADEMA itaendelea kupinga vitendo vya rushwa katika siasa na kwamba chama hicho kitazidi kuwasimamia wananchi kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kukataa kununuliwa dhamira yao ya kisiasa na kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko ya kweli nchini.