
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaid Khamis, amewataka wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Zanzibar, hususani katika sekta ya utalii, uchumi wa buluu na biashara, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Siku ya Zanzibar, Mwanaidi amesema wanawake wana nafasi kubwa ya kuchangia ustawi wa uchumi ikiwa watatumia ipasavyo mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa visiwani humo.
Siku hiyo maalumu imewakutanisha Wazanzibari waliokuja kuonesha utamaduni wao, bidhaa za asili pamoja na kutangaza maeneo ya biashara na uwekezaji kupitia miradi ya ubia, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha fursa za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis, amesema tukio hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali na Wazanzibari, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika biashara na uchumi.