
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Tanzania bara Stephen Wasira amewataka wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kwa ngazi ya wilaya kupitisha wagombea ubunge wanaokubalika kwa wananchi mchakato wa kura za maoni utakapoanza.
Wasira ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu za CCM ndani ya mkoa wa Geita kupitia vikao vya ndani mkoani humo.

Amesema baadhi ya watia nia wa nafasi za ubunge hutumia fedha kuwahonga wajumbe na kwamba chama hicho hakipo tayari kupitisha wagombea wanaotanguliza fedha badala ya sera thabiti za kuwatumikia wananchi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Geita Nikolaus Kasendamila amewahakikishia wananchi wa mkoa huo kuwa CCM itapitisha wagombea wenye sifa na weledi watakao shughulikia matatizo ya wapiga kura wao.