Jeshi la Polisi Mkoani Tabora limetangaza kuwashikilia watu watatu kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa wametekwa ili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa ndugu na wana familia wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao amewaambia waandishi wa habari kuwa watuhumiwa wanaoshikiliwa ni Khadija Jimmy Murijo (39)- kabila Mpare ambaye pia ni mke wa Bw. Emmanuel Peter Mchali, Ashura Swalehe (48) na Vitus Joseph (34) ambapo wote wanadaiwa kushirikiana kutengeneza taarifa ya uongo kwamba Khadija Jimmy ametekwa na watu wasiojulikana.
Watuhumiwa hao inaelezwa kuwa walitengeneza uongo huo ili kujipatia fedha kwa mume wa Khadija Murijo, ambapo walijipatia kiasi cha shilingi 1, 385, 800 kati ya Shilingi Milioni 2 walizoziamrisha kuzipata kutoka kwa Bw. Emmanuel.
Awali walieleza kuwa Khadija alikuwa ametekwa huko Ulyankulu na katika uchunguzi uliofanyika ulibaini kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa ameenda Wilaya ya Urambo, Kijiji cha Vumilia na baada ya uchunguzi inaonekana fedha hizi zote walizitolea kwenye wilaya ya Kaliua.
“Uchunguzi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.” Amesema Kamanda Abwao.
Kwa upande wake mume wa Khadija, Bwana Emmanuel Peter Mchali amesema siku hiyo alipigiwa simu na mke wake na kumueleza kuwa ametekwa na kupata vitisho kutoka kwa mwanaume mmoja kupitia simu ya mkewe, wakimtaka atoe milioni mbili ili kuweza kuachiwa kwa mkewe, suala ambalo lilimlazimu kukopa fedha ili kwenda kulipa kwa watuhumiwa hao.