Naomi Milton- KIGOMA
Watumishi sita wa Idara ya Afya halmashauri ya wilaya ya Kigoma wamefariki dunia baada ya boti waliokuwa wakiitumia kupinduka na kuzama ndani ya Ziwa Tanganyika wakati wakieleka kusambaza dawa katika vijiji vilivyopo mwambao wa ziwa hilo.
Akithibisha kutokea kwa tukio hii leo Mkuu wa wilaya ya Kigoma Rashid Chuachua amesema jumla ya watumishi 18 walikuwa ndani ya boti ambapo watu sita wamefariki dunia majeruhi tisa wameokolewa na kukimbizwa hospitali huku watatu wakiendelea kutafutwa.

DC Chuachua ameongeza kuwa watumishi hao walitumia boti ya halmashauri ya wilaya kwenda kijiji cha Kagunga kwa ajili ya chanjo na dawa mbalimbali lakini kutokana na hali mbaya ya hewa na upepo mkali ulioambatana na mvua ilisababisha boti hiyo kupinduka.
Hata hivyo juhudi za uokoaji bado zinaendelea katika eneo hilo huku vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wakiendelea kuwatafuta watu watatu ambao hawajapatikana hadi sasa.

