
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa majiko na mitungi ya gesi 486 kwa watumishi wote wa magereza manane ya mkoa wa Kagera ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono sera ya serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania wote ifikapo 2034.
Akizindua zoezi hilo kwa watumishi 99 wa magereza ya Bukoba kwa niaba ya mwenyekiti wa bodi ya REA Bw. Lucas Charles amesema kuwa serikali imeshaziagiza magereza zote nchini kuhamia katika matumizi ya nishati safi.
Lucas amesema lengo la kugawa majiko hayo na mitungi ya gesi ni kutaka kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya mkaa na kuni ili kulinda mazingira na kuepuka matatizo yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.
Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Magereza ambaye ni Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Heron Norbert amesema kuwa tayari magereza zote za mkoa huo zimeanza kutumia nishat safi na kuahidi kuwa watumishi wa magereza Bukoba wataenda kuwa mabalozi juu ya matumizi ya nishati safi.