Naibu Waziri wa Madini Steven Kiruswa ametoa rai kwa wawekezaji katika sekta ya madini kuweka wazi taarifa za tafiti kuhusu madini kwa wananchi ili wanufaike na shughuli za uchimbaji kwenye maeneo mbalimbali yanayowazunguka.
Kiruswa amesema hayo February 24, 2026 Bukombe Mkoani Geita wakati akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ushirikiano wa uchimbaji madini kati ya Shirika la Madini la Taifa STAMICO na Kampuni ya Uchimbaji dhahabu ya Plantcor ya nchini Afrika Kusini.
Amesema ni muhimu tafiti kuhusu madini zifanyike kwa teknolojia ya kisasa kuepusha uharibifu wa mazingira na kuwakumbusha wawekezaji wote wajibu wao wa kurudisha kwa jamii (CSR).
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Plantcor Bwn. Joseph Wilmans ameahidi kuzingatia uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika tafiti na shughuli zote za uchimbaji madini Wilayani Bukombe kulingana na maelekezo ya Serikali
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amehimiza wabia hao kuzingatia Sheria na taratibu za nchi katika sekta ya madini kwa masilahi ya wananchi na Taifa

Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita Dkt. Dotto Mashaka Biteko amesema maendeleo katika sekta ya madini Wilayani humo yamesaidia kupunguza Uharifu ambao awali ulijenga hofu kwa wawekezaji
Mkataba huo wa ushirikiano katika sekta ya madini kati ya STAMICO na Kampuni ya Plantcor unalenga kufanya tafiti na uchimbaji madini katika msitu wa Kigori uliopo Wilayani Bukombe wenye ukubwa wa Kilomita za mraba 7,460
