
Halmashauri ya manispaa ya Bukoba mkoani Kagera imetakiwa kuwatafuta wawekezaji kwenye fukwe za ziwa Victoria ili kukabiliana na changamoto ya uchafuzi uliokithiri wa fukwe hizo unaotokana na utupaji wa taka hovyo.
Hayo yameelezwa na afisa mkoani Kagera Yassin Mwinori wakati akiongea na redio Kwizera na kwamba uchafuzi wa fukwe hizo ambao unatokea mara kwa mara unatokana na baadhi ya wananchi wanaotembelea fukwe hizo kushindwa kuhifadhi taka wanazokutana nazo.
Amesema kuwa mbali na kutafutwa kwa wawekezaji pia idara ya afya inao mpango wa kuweka vifaa vya uhifadhi wa taka lakini pia kuwa na siku moja kwa wiki ya kufanya safi fukweni na kuiomba jamii kuheshimu na kulinda mazingira ya fukwe.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa manispaa ya Bukoba akiwemo Abdul Shaaban na Theonistina Kasharo wamesema kuwa changamoto ya uchafuzi wa fukwe inatokana na kukosekana kwa vifaa vya kuhifadhi taka na kwamba suala kuwaweka wawekezaji itasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti uchafuzi kwani eneo hilo litakuwa na uangalizi.