Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki EACOP kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Chonolean Tanga umefikia asilimia 79 na utakamilika Julai 2026.
Akizungumza leo Jan. 05 ,2026 Jijini Dar es Salaam, katika mkutano na waandishi wa habari, kufuatia ziara ya viongozi wa Uganda kutembelea mradi wa EACOP, Ndejembi amesema mradi huo ni muhimu kwa Tanzania na Uganda.
Kukamilika kwa mradi huo ni baada ya karibu miaka 10 ya utekelezaji wake unaohusisha ujenzi wa bomba la inchi 24 lenye urefu wa kilomita 1,443 likiwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi.
Mradi huo upo chini ya wanahisa Kampuni ya Total Energy yenye hisa asilimia 62, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanznaia (TPDC) asilimia 15, UNOC asilimia 15 na CNOOC asilimia 8.
Amesema Tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2016 Serikali ya Tanzania imewekeza fedha nyingi kuhakikisha unakamilika kwa wakati kwa manufaa ya taifa.