
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepokea vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 91,000 (Sh milioni 240) kwa ajili ya kuimarisha juhudi za kudhibiti ujangili na wanyamapori wakali na waharibifu nchini.
Vifaa hivyo ni pamoja na pikipiki 20 na ndege nyuki (drones) saba vimetolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara (IWT), na kukabidhiwa rasmi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.
Aidha, Waziri Chana alibainisha kuwa utekelezaji wa Mradi wa IWT umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la idadi ya tembo nchini kutoka 43,000 mwaka 2014 hadi zaidi ya 60,000 mwaka 2022, jambo linaloonesha mafanikio ya dhahiri ya mikakati ya Serikali katika kulinda rasilimali za taifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dk. Fortunata Msoffe, amesema Mradi wa IWT umeimarisha vikundi vya doria (TCGs), kutoa mafunzo ya uhifadhi, kutumia taarifa za kiintelijensia, na kukuza ushirikiano baina ya taasisi za ulinzi na uhifadhi nchini.
Naye Mwakilishi wa UNDP, Godfrey Mulisa, amesema UNDP inaunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, hususan katika kukuza utalii na kukabiliana na ujangili wa wanyama pori na biashara haramu ya nyara.
Mradi huu pia umechangia kutatua migogoro baina ya binadamu na wanyama pori kwa kuanzisha miradi ya kijamii ya kuinua kipato ikiwemo ufugaji wa nyuki, kilimo salama na shughuli jumuishi za kijinsia.