
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax amesema uwepo wa ushirikiano wa kidiplomasia wa kiulinzi kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na majeshi ya nchi zingine umesaidia watu aliowataja kutaka kufanya vurugu nchini kutoungwa mkono na nchi zao.
Dkt. Stergomena ameyasema hayo Mei 22, 2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari na kutabainisha kuwa nchi hizo zimekuwa mstari wa mbele kuitetea Tanzania.
Amesema kuwa watu walitegemea kuona nchi za watu waliojipenyeza nchini zikiwaunga mkono watu wao lakini nchi hizo hazikufanya hivyo kutokana na ushirikiano wa kidiplomasia.
Aidha Dkt. Stergomena amesema wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inajivunia mafanikio katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo usalama wa miradi ya kimkakati na kuchangia kujenga uchumi.
Amesema pia, bajeti ya wizara hiyo imeongezeka kutoka Sh trilioni 2 mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh trilioni 3.6 mwaka wa fedha 2025/26 na huduma za afya zikiimarishwa na asilimia 80 ya wanufaika wa huduma hizo ni raia.