Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema vurugu na uharibifu uliotokea nchini wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, unaweza kuipunguzia sifa Tanzania kupata mikopo na misaada mbalimbali kutoka kwenye Taasisi za Kimataifa.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo November 18, 2025 mara baada ya kuwaapisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa serikali ya awamu ya Sita Ikulu, Chamwino Mjini Dodoma, akiwataka Mawaziri kujipanga katika utafutaji wa fedha na matumizi ya rasilimali zilizopo ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha Rais Samia amekiri kuwa rasilimali za Taifa ni chache suala ambalo limeifanya Tanzania kuwa tegemezi wa Mikopo kutoka nje.
Katika hatua nyingine Rais Samia amesisitiza kuwa majukumu na dhamana alizotoa kwa Mawaziri na Manaibu mawaziri hao ni dhamana za kazi na sio fahari, akiahidi kufuatilia mienendo yao katika kutimiza kaulimbiu ya serikali yake ya ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’.
“Dhamana zetu ni dhamana za kazi na si fahari kwamba na mimi ni Waziri ikawa ndio fahari ulipotoka, unapokaa na kwingineko. Tumebeba majukumu ya kwenda kuwatumikia wananchi. Utu uanze na sisi wenyewe viongozi ambao tunaenda kuwasimamia wengine.” Ameeleza.
Rais Samia katika hotuba yake amesema kazi kubwa kuanzia leo kwa wateule hao ni kuwajibika kwa wananchi na kwa Taifa, akisema ahadi kwa wananchi ni nyingi mno na muda wa kutekeleza ni mchache, akiwataka wale wazito wa mwili kupunguza kilo zao ili kuendana na kasi anayoitaka katika kutimiza ahadi zake kwa wananchi.