
Na Samuel Samsoni- Kahama, Shinyanga
Zaidi ya dira za maji 400 zimeibiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kwa kipindicha mwezi Oktoba mpaka July 2025 na kusababisha hasara ya zaidi ya Shilingi milioni 40
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama imetahadharisha juu ya mwendelezo wa wizi za dira za maji (mita) ambao umekuwa ukiendelea bila kufahamu ni wapi zinapopelekwa na nani mhusika mkuu wa mchakato huo.
Kipindi cha Mchakato cha Radio Kwizera kilifika katika Ofisi za Ofisa Mahusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama na kuzungumza na Ofisa Mahusiano John Mkama ambaye amekiri kuwa mita hizo zimeibiwa kwa kipindi cha tangu Oktoba mwaka 2024 mpaka Julai mwaka huu licha ya juhudi za kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi lakini bado hakujazaa matunda.
“…hivi ninavyoongea jana tulikuwa na kikao na Mkuu wa polisi Wilaya ya kipolisi Kahama OCD Mtaju Mayombo kujadili suala hili na namna ya kulikabiri janga hili kwa nguvu zote, lakini pia tumewashirikisha viongozi wa Sungusungu ili kutusaidia kuimarisha ulinzi katika maeneo yao” Amesema Mkama.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja kutoka Mamlaka hiyo Bw. Gantala Hawaiju amesema katika kuwafikishia wananchi huduma, Mamlaka inakumbwa na athari ambazo zinasababishwa na wizi wa mita.
“… Athari tunazokutana nazo kwanza ni hasara ya mita, lakini hasara ya pili ni maji kwani wanapoiba wanaacha maji yakiendelea kumwagika, lakini hasara ya tatu ni bili ya mteja ambayo wakati mita inaibiwa mteja alikuwa ametumia maji na mita ikaibiwa kabla ya mamlaka kusoma bili hizo lakini hasara kubwa ni kumuacha mwananchi akiwa hana huduma ya maji na pengine hana fedha nyingine itakayomuwezesha kununua mita nyingine kwa wakati huo” Amesema Bw. Hawaiju.
Hata hivyo baadhi ya wananchi Jovina Mathias na Deodatus Michael wameomba hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa ili kukomesha wizi wa mita katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.