
Hospitali Teule ya Mugana iliyopo wilaya ya Misenyi mkoani Kagera imeibuka mshindi katika mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2024 kwa upande wa hospitali za wilaya.
Nafasi ya pili imeshikwa na Hospitali ya Mji wa Njombe (Kibena) huku ya tatu ikikamatwa na Hospitali ya Wilaya Chunya iliyopo mkoani Mbeya.
Mashindano hayo yanaandaliwa na kuendeshwa na Wizara ya Afya ambapo mshindi katika vipengele mbalimbali hupatikana kwa uhakiki kufanyika kwa kuangalia ufikiaji wa vigezo mbalimbali.
Vigezo hivyo ni pamoja na utunzaji na upendezeshaji wa mazingira, upatikanaji wa maji, udhibiti wa taka, matumizi ya vyoo bora kwenye kaya, maeneo ya biashara na taasisi.
Wizara ya Afya kupitia taarifa yake ya orodha ya washindi imeeleza kuwa mwaka 2024 mashindano hayo yalikuwa yakihusisha halmashauri za majiji, halmashauri za manispaa, halmashauri za miji, halmashauri za wilaya, halmashauri za vijiji, Halmashauri za mitaa, vyuo vikuu, hospitali za wilaya, hospitali za rufaa za mikoa, shule za msingi na shule za sekondari.