Watu 12 wanahofiwa kufariki dunia baada ya ndege ndogo aina ya Cessna Caravan yenye nambari ya usajili 5Y-CCA kuanguka katika eneo la pwani la Kwale wakati ikielekea Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara, nchini Kenya.
Ajali hiyo imetokea leo October 28, 2025 katika eneo lenye milima na misitu takriban kilomita 40 kutoka uwanja wa ndege wa Diani.
Kamishna wa Kaunti ya Kwale, Stephen Orinde ameliambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo ni watalii wa kigeni.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya (KCAA) Emile Arao amethibitisha kwamba ndege hiyo, iliyokuwa na watalii 12 ilikuwa ikielekea Kichwa Tembo eneo la Maasai Mara na uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali unaendelea.
Mashuhuda waliiambia AP kwamba walisikia mlipuko mkubwa, na walipofika eneo la tukio walikuta mabaki ya miili ambayo haikutambulika.
Aidha Shirika la ndege la Mombasa Air Safari liliiambia AP kwamba linashirikiana na mamlaka ya usafiri wa anga na taarifa kuhusu ajali hiyo zitatolewa kupitia mamlaka hiyo.