Kongamano kuhusu Nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika kufanikisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2026/2027–2030/2031 linaendelea hivi sasa katika Taasisi ya Confucius, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kongamano hili lililoandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) limewaleta pamoja wadau mbalimbali, ikiwemo viongozi wa sekta ya umma na binafsi, Wataalamu wa uchumi, na wabunifu wa miradi ya maendeleo, ambao wanajadili jinsi PPP inavyoweza kuchochea uwekezaji, kuimarisha miundombinu na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya taifa.
Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji ameshiriki Majadiliano hayo yaliyojikita katika kutafuta njia bora za kuimarisha ushirikiano, kuongeza ufanisi wa miradi ya maendeleo, pamoja na kuweka mazingira wezeshi yatakayovutia uwekezaji zaidi kupitia mfumo wa PPP
Imeelezwa, kongamano hilo ni fursa ya kipekee kwa Wadau kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kufanikisha malengo makuu ya maendeleo ya taifa.
