
Uongozi wa timu ya Junguni United inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar (PBZ) umewafukuza wachezaji saba wa timu hiyo kwa tuhuma za kujihusisha na michezo ya kubashiri matokeo ya mchezo (betting).
Wachezaji hao walibeti katika michezo miwili waliocheza na Malindi pamoja na New City.
Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Junguni, Suleiman Mwidani ambaye amesema, wachezaji hao wamevunja katiba ya klabu hiyo na kukiuka kanuni ya Ligi Kuu ya Zanzibar ya 2024/25, kifungu namba mbili na tatu, sura ya 23.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, baada ya viongozi kufanya uchunguzi na kujiridhisha wamewasimamisha wachezaji hao kujihusisha na shughuli yoyote inayohusu timu hiyo na kucheza mpira wa miguu.
Pia, viongozi hao waliliomba Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF) kuwapa adhabu, ili kukomesha michezo ya bahati nasibu kwa wachezaji wenye nia ya kurudisha maendeleo ya soka kisiwani hapa.
Wachezaji hao saba waliosimamishwa kwa tuhuma hizo ni; Salum Athumani ‘Chubi’, Ramadhan Ally Omar ‘Matuidi’, Abdallah Sebastian, Danford Mosses Kaswa, Bakari Athumani ‘Jomba Jomba’, Rashid Abdalla Njete na Idd Said Karongo.