
Timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) imefanikiwa kusuluhisha mgogoro wa mpaka baina ya majirani wawili uliodumu kwa miaka mitano.
Mgogoro huo uliosuluhishwa jana April 27, 2025 ulikuwa kati ya Bw. Sadock Bitungwa na Bw. Telesphory Emmanuel wakazi wa kijiji cha Ruganzo kata ya Kibimba wilayani Ngara mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Bw. Telesphory amesema licha ya juhudi za usuluhishi katika ngazi za kata na wilaya jambo hilo halikufanikiwa huku Bw. Sadock akikubali mgogoro baina yao uishe ili kuwe na amani.
Bi. Mary Jeremiah jirani wa Bw. Sadock na Telesphory amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuja na msaada huu wa kisheria hasa kwa wananchi wa kawaida jambo lililosaidia kuleta amani miongoni mwa majirani zake.
Aidha zoezi la uwekaji alama za mpaka baina ya majirani hao limesimamiwa na viongozi wa kijiji, kata, Afisa Ardhi wilayani Ngara Bw. Cosmas Rubambura pamoja na Mratibu MSLAC kwa wilaya ya Ngara kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili Mwanaidi Msangi.
Ikumbukwe timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya ‘Mama Samia Legal Aid’ inatarajia kuhitimishwa leo April 28, 2025 ambapo itakuwa imevifikia vijiji 45 ndani ya kata 15 za wilaya ya Ngara ili kutoa elimu na msaada wa kisheria.