
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amesema jumla ya wanafunzi 214,141 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya elimu ya ufundi kwa mwaka wa masomo 2025.
Kati yao, wasichana ni 97,517 na wavulana 116,624.
Wanafunzi hao ni miongoni mwa waliokamilisha Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2024, wakiwemo wanafunzi kutoka shule za Serikali, zisizo za Serikali, pamoja na watahiniwa wa kujitegemea.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi 149,818 (asilimia 69.96 ya waliochaguliwa) wamepangiwa kujiunga na kidato cha tano katika shule 694 za sekondari za Serikali.
Miongoni mwao, wasichana ni 76,491 na wavulana 73,327.
Aidha, wanafunzi 2,875 (wasichana 1,057 na wavulana 1,818) wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vinne vya elimu ya ufundi.
Vyuo hivyo ni Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo cha Maendeleo ya Maji (WMDI).
Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa uchaguzi huu umezingatia viwango vya ufaulu na nafasi zilizopo, hivyo hakutakuwa na mabadiliko ya shule au chuo kutokana na ukosefu wa nafasi.
Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano utaanza rasmi Julai 8, 2025, huku muda wa kuripoti ukiwa kuanzia Julai 6 hadi Julai 21, 2025. Kwa wanafunzi wa vyuo, maelekezo ya kujiunga yatatolewa na taasisi husika.