
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa licha ya hali ya uchumi duniani kuendelea kuyumba, Tanzania imeonyesha uimara kwa kuendelea kukuza uchumi wake kwa kasi na ustahimilivu wa hali ya juu.
Prof. Mkumbo ameeleza hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akitoa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2024/2025 na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2025/2026.
Amesema kuwa Kuimarika kwa uchumi kunatokana na usimamizi makini wa sera za uchumi jumla, pamoja na ushiriki wa wananchi wote katika ujenzi wa Taifa.
Aidha Prof. Mkumbo amebainisha kuwa licha ya changamoto za kiuchumi duniani, Tanzania imeendelea kuvutia wawekezaji na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu, nishati, kilimo na afya hatua ambazo zimechangia ustawi wa uchumi wa Taifa
Aidha Prof. Mkumbo amesema Pato la Taifa linatarajiwa kuendelea kupanda hadi asilimia 6.0 mwaka 2025 na kufikia asilimia 6.1 mwaka 2026, akisisitiza kuwa msingi wa mafanikio haya ni utekelezaji thabiti wa sera bora za uchumi na ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya Taifa.
Amesema Katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2024, Pato Halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 5.6 ikilinganishwa na asilimia 5.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2023