
Jumla ya watumishi wa umma 172 katika halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita wamebainika kuwa na utata wa tarehe za kuzaliwa katika vyeti vyao ambapo serikali imeagiza vyombo husika kuwafanyia uchunguzi.
Agizo hilo limetolewa na kaimu mkuu wa mkoa wa Geita Bi. Fatma Mwassa ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Kagera kupitia kikao cha Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG kilichofanyika katika halmashauri hiyo.
Amesema haiwezekani zaidi ya watumishi 100 wa halmashauri moja wote vyeti vyao vikosewe tarehe ya kuzaliwa na kwamba kuna kila sababu ya kufanya uchunguzi wa kina na atakaebainika kukiuka sheria achukuliwe hatua.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato Christian Manunga ameahidi kutoa ushirikiano katika uchunguzi huo huku akieleza kuwa kwa kipindi cha miaka 10 wamepata hati safi na isiyo na mashaka.