
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, leo Alhamisi Juni 26, 2025, ametoa hotuba ya kuhitimisha Mkutano wa 19 wa Bunge la 12, huku akimkumbuka hayati Rais John Magufuli na kumsifu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza vyema licha ya kuachiwa nchi katika kipindi kigumu baada ya kifo cha Magufuli.
Katika hotuba yake amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wake, Rais Dkt. Samia ameweza kusimama imara katika kuendeleza miradi ya kimkakati na huduma za jamii, kusimamia demokrasia, kujenga uchumi na kuimarisha diplomasia.
Amesema Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa Mwalimu wa subira, kielelezo cha ujasiri, ustahimilivu na alama ya matumaini kwa kizazi hiki na kwmba ni kiongozi aliyetoa mfano wa kuwa mwanamke anaweza kuongoza hata kwenye nafasi ya Kitaifa.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kutokana na uongozi dhabiti wa Rais Dkt. Samia, taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa zimetambua mchango na maono yake katika kusimamia shughuli za kimaendeleo nchini na kuitangaza Tanzania nje ya nchi.
Ameongeza kuwa jitihada za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika nyanja mbalimbali zimetoa msukumo kwa wanazuoni katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya Tanzania kumtunuku Shahada ya Juu ya Udaktari wa Heshima.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza watendaji wote wa Serikali kwa kutekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia na kwamba leo tunajivunia mafanikio makubwa katika utendaji wa Serikali kwa kila sekta hapa nchini, Mafanikio hayo yanatokana na kujitoa kwao katika kuhakikisha mikakati na maono vinatekelezwa kama ilivyokusudiwa