
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameelekea nchini Belarus kwa ziara rasmi ya kikazi ya siku tatu, ziara inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kukuza fursa za kiuchumi kati ya Tanzania na Belarus.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin ambapo watajadili masuala ya ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu,Kilimo na viwanda.
Waziri Mkuu pia atapata fursa ya kutembelea kiwanda kikubwa cha kutengeneza dawa nchini humo cha Republican Unitary Production Enterprise na kujionea mbinu za kisasa za uzalishaji wa bidhaa za afya.
Pia, atatembelea kiwanda cha matrekta cha Minsk Tractor Works JSC pamoja na chuo kikuu cha Agrarian State University, na anatarajiwa kufanya mikutano ya uwili itakayojumuisha viongozi wa kiserikali na Chama cha wafanyabiashara wa Belarus cha AFTRADE.
Lengo la mikutano hiyo ni kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kuvutia wawekezaji kutoka Belarus kuja kuwekeza Tanzania katika sekta za kimkakati.