
Mtoto Ramin Ahmed mwenye umri wa miaka 3, aliyekuwa anaishi na wazazi wake eneo la Malabi, Kata ya Mpela mkoani Tabora, amepatikana akiwa amefariki dunia katika Kisima kilichopo nyumba waliyokuwa wakiishi.
Awali, familia ya mtoto huyo ilisambaza taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikitangaza kumzawadia Sh10 milioni yeyote mwenye taarifa alipo mtoto wao.
Akizungumzia tukio hilo, leo Jumatatu Julai 21, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha kupatikana kwa mtoto Ramin akiwa tayari amefariki ndani ya kisima.
Amesema Julai 18, 2025 saa mbili usiku Ramin alikuwa akicheza na wenzake kwenye kokoto nje ya nyumba yao wakati mama yake akiendelea kupanga vitu walivyokuwa wanahamisha kwenda nyumba nyingine ambapo baada ya muda hakumuona mtoto wake.
Kamanda huyo amewahimiza wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuweka visima mifuniko pia kuvijengea ili kuepusha majanga kama hayo ambayo yanagharimu uhai wa watoto na haipaswi watoto kucheza karibu na visima vya maji.