
Mkutano Mkuu wa 20 wa Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu Kanisa Katoliki wa Afrika na Madagaska (SECAM) umewasihi viongozi wote wa kisiasa kutumia mazungumzo kama njia bora ya kutafuta amani maeneo yenye changamoto za amani.
Katika waraka uliotolewa na Makardinali, Maaskofu wakuu, na Maaskofu, washiriki wa SECAM kwenye hitimisho la mkutano huo Jijini Kigali nchini Rwanda jana umetamka kuwa Upatanisho, msamaha, na amani ni mambo muhimu kwa maendeleo ya nyanja zote za maisha ya mwanadamu.
Aidha wamesema kuwa Kanisa, kama shahidi wa mateso ya watu katika maeneo yanayokumbwa na vita, lazima lijitoe kwa nguvu zaidi katika kukuza ufahamu na kuchukua hatua madhubuti kwa ajili ya amani.
Rais wa Mabaraza ya Maaskofu wa SECAM, Kardinali Fridolaa Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa, amewahakikishia washiriki na waumini kwa ujumla kwamba Afrika ina kila sababu ya kuwa na matumaini kuhusu mustakabali wake.