
Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) leo kinatarajia kuwateua wagombea urais wa Tanzania na Zanzibar katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa chama hicho ambao pia utateua mgombea mwenza wa urais wa Tanzania na mgombea mwenza wa urais wa Zanzibar.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano na Taarifa kwa Umma, John Mrema imeeleza kuwa mkutano huo unafanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Mrema amesema pia, katika mkutano huo chama hicho kinatarajia kuzindua Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030 ambayo inatokana na sauti ya wananchi na mahitaji ya taifa kwa sasa.
Aidha CHAUMMA kimesema hadi kufikia Agosti 4, mwaka huu kimepata jumla ya watia nia wa udiwani 2,116 kati ya kata 3,953, sawa na asilimia 53 ya kata zote nchini.
Aidha, kwa upande wa ubunge, CHAUMMA imesema ina watia nia 183 kwenye majimbo 162 kati ya majimbo 222, sawa na asilimia 70 ya majimbo yote Tanzania Bara.