
Viongozi 32 wa Vyama vya Ushirika wa Wakulima wa Pamba (AMCOS) katika Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, wamekamatwa kwa tuhuma za kuchezea mizani za kielektroniki ili kuiba sehemu ya pamba ya wakulima.
Tukio hilo limebainika kupitia operesheni maalum inayoendelea nchini, ambapo kwa upande wa Igunga pekee viongozi hao wanadaiwa kuiba zaidi ya kilo 900,000 za pamba katika kipindi cha msimu huu wa masoko.
Akizungumza na wakulima na viongozi wa zao hilo wilayani humo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha, ameagiza viongozi hao kukamatwa papo hapo na kufutwa kazi mara moja, akisisitiza kuwa makosa yao hayawezi kuvumilika kwa maslahi ya mkulima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo za Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Samson Poneja, ameagiza AMCOS zote nchini kuhakikisha mizani inahakikiwa na Wakala wa Vipimo, akisisitiza umuhimu wa kufanya uhakiki hasa wakati wa msimu wa masoko ili kulinda maslahi ya wakulima.