
Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, imesema usiri wa mawasiliano kati ya mshtakiwa na wakili wake ni haki ya msingi, lakini una mipaka ili kulinda usalama wa mshtakiwa na gereza.
Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Elizabeth Mkwizu kupitia Naibu Msajili Livin Lyakinana, katika shauri la Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu,Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye aliomba asiguswe na askari Magereza wala nyaraka zake zisiguswe akiwa mahakamani.
Jaji Mkwizu amesema mshtakiwa hapaswi kuzuiwa kuwasiliana na wakili au kupokea nyaraka bila sababu, lakini Magereza wana wajibu wa kumlinda mshtakiwa na pia, nyaraka zinaweza kukaguliwa kwa mujibu wa sheria.
Mahakama imetupilia mbali ombi la Lissu kupinga mashahidi kufichwa katika kesi yake ya madai ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, ikisema hoja hizo hazina mashiko kisheria.
Aidha, Jaji Mkwizu amesema kiapo cha Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam, ACP Faustine Mafwele, kinajitosheleza kisheria na kina taarifa rasmi, hivyo si lazima kuwe na viapo vya mashahidi waliodai kutishiwa.
Kuhusu madai kwamba hakupewa haki ya kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Geofrey Mhini, Mahakama Kuu imesema hakimu huyo alizingatia haki hiyo.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kuwatuhumu askari Polisi kuiba kura na majaji kutokutenda haki ili wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.