
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa OR-TAMISEMI kwa kushikiana na Wadau wa Sekta ya Afya imekabidhi seti ya vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya (WAJA) 3,561 waliohitimu mafunzo ya kutoa huduma za afya ngazi jamii.
Hayo yamejiri jana kupitia hafla fupi ya utoaji wa vyeti kwa wahitimu 222 katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, wakiwakilisha kundi la Wahudumu 3,561 awamu ya kwanza ya wahudumu waliohitimu mafunzo hayo katika mikoa 12.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omary Jiri, akizungumza kwenye hafla hiyo amesema Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya karibu zaidi na wananchi na sasa tunashuhudia wahudumu hawa wa afya ngazi ya jamii wamehitimu na wapo tayari kwa ajili ya kuanza kazi wakiwa na nyenzo zote muhimu kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema Wahudumu hao huchaguliwa na wananchi katika maeneo yao wanayoishi ambapo kila kitongoji au mtaa huchagua watu wawili, mwanaume na mwanamke ambao Wizara huwapatia mafunzo ya darasani kwa muda wa miezi mitatu na miezi mitatu mafunzo kwa vitendo katika jamii.