
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Iman Njalikai amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Algeria (Sonatrach), Rachid Hachichi kwa lengo la kujadili fursa za uwekezaji na ushirikiano katika sekta za mafuta na gesi asilia baina ya mataifa hayo.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Iman amesema Tanzania na Algeria zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi katika maeneo mbalimbali, lakini kwa mara ya kwanza mazungumzo yanafanyika kwa kuhusisha PURA.
Amesema Tanzania inaendelea kujenga uwezo wa wataalamu wake wakiwemo wanaofanya kazi PURA, hivyo kuiomba Sonatrach kuendelea kutoa fursa za mafunzo na programu za kujenga uwezo.
Balozi Iman pia ameikaribisha Sonatrach kuwekeza katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania hususan katika vitalu vya utafutaji wa mafuta mara baada ya zoezi la kunadi vitalu kuzinduliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Sonatrach, Rachid Hachichi amesema kampuni hiyo ipo tayari kutumia fursa na kuendelea kushirikiana na taasisi za Tanzania ikiwemo PURA katika kujenga uwezo wa wataalamu katika masuala ya mafuta na gesi asilia.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Algeris, Algeria na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa Sonatrach na ujumbe kutoka Tanzania uliojumuisha viongozi na maafisa waandamizi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).