
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameongoza uzinduzi wa Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara hatua inayolenga kusaidia uwezeshaji wa wafanyabiashara katika ngazi zote.
Akizungumza Septemba 10, 2025 wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mhita amesema dawati hilo limeanzishwa na TRA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kwa lengo la kuwatambua, kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyabiashara ili kukuza mitaji na kuongeza tija katika biashara zao.
Mhita amebainisha kuwa dawati hilo litakuwa daraja la kuwaunganisha wafanyabiashara na taasisi za kifedha ili kupata mikopo kwa urahisi zaidi pamoja na kuwaongoza katika njia bora za urasimishaji biashara.