
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeliondoa jina la Luhaga Mpina, mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, kwenye orodha ya wagombea wa kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huo wa INEC unafuatia pingamizi lililowasilishwa na Hamza Johari, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, dhidi ya uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imefikia uamuzi huo katika kikao chake kilichofanyika leo Septemba 15, 2025, kikao kilichoketi kwa lengo la kutoa uamuzi wa mapingamizi manne yaliyowasilishwa kwa nafasi ya Urais ambapo mapingamizi matatu yamekataliwa na moja limekubaliwa.
Mapingamizi yaliyokataliwa na kutupiliwa mbali lile lililowekwa na Almas Hassan Kisabya mgombea wa kiti cha Urais kupitia Chama cha NRA dhidi ya Luhaga Mpina, mgombea wa kiti cha Urais kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, na pingamizi lililowekwa na Kunje Ngombale Mwiru, mgombea wa kiti cha Urais kupitia chama cha AAFP dhidi ya Luhaga Mpina, mgombea wa Kiti cha Urais kupitia Chama cha ACT- Wazalendo
Pingamizi lingine lililokataliwa ni lile lililowekwa na Luhaga Mpina, mgombea kupitia Chama cha ACT-Wazalendo dhidi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pingamizi lililokubaliwa ni lile lililowasilishwa na Hamza Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.