
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ametoa wito kwa wananchi wote wenye umri wa kuanzia miaka 18 ambao wamekosa elimu ndani ya mfumo rasmi kutumia fursa ya uwepo wa vituo vya elimu ya watu wazima kupata maarifa na ujuzi.
Ametoa wito huo tarehe 15 Septemba, 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya juma la Elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi Mkoa wa Mwanza yaliyofanyika uwanja wa Sabasaba Wilayani Magu
Amesema, Mkoa huo una zaidi ya watu 262,500 ambao hawajui kusoma na kuandika na kwamba serikali imeanzisha vituo katika Halmashauri zote nane ambapo kuna zaidi ya wanafunzi elfu 36 wanaopatiwa elimu nje ya mfumo rasmi hivyo ni fursa ya kukimbilia kwa wote waliokosa.
Mtanda amebainisha kuwa elimu ya watu wazima inajumuisha programu mbalimbali ikiwemo MEMKWA ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuwawezesha waliokosa elimu ya msingi kupata stadi za kujua Kusoma, kuhesabu na kuandika ili kufuta ujinga.
Aidha, amebainisha kuwa ndani ya mfumo huo kipo kipengele cha MUKEJA ambacho kinatoa fursa ya kutoa maarifa kwa uwiano ambapo jamii inapewa stadi za ujuzi mbalimbali za ujasiriamali na akabainisha kuwa kuna zaidi ya wafungwa 300 mkoani humo wanapatiwa elimu hiyo.
Akitoa taarifa ya Mkoa Mkurugenzi Msaidizi wa Taaluma – TEWW, Dkt. Onesmo Nyamweru amesema juma jilo linaadhimishwa kila mwaka jirani na tarehe 8 septemba kwakua ndiyo siku ya Kisomo cha Kimataifa ulimwenguni kote na kwamba maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kutafakari dhana na maendeleo ya Programu za elimu ya watu wazima kupitia maendeleo ya teknolojia.
Dkt. Nyamweru amesema elimu nje ya mfumo rasmi kitaifa imepanda kutoka 78% hadi 83% na kwa Mwanza wanaojua kusoma na kuandika ni 85.6% elimu hii ni nyenzo muhimu ya kupambana na umasikini, ujinga na maradhi na inakidhi mahitaji ya watu wazima ya sasa kwa jamii iliyo katika shughuli za uzalishaji mali.