
Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Juma Mpuya mwenye umri wa Miaka 45, mlinzi wa maduka ya mfanyabiashara amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana katika eneo lake la kazi Mjini Shinyanga.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Septemba 17, 2025, katika mtaa wa Majengo Mapya, kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mwili wa marehemu ulikutwa umefungwa sehemu za mikono na miguu, huku baadhi ya mali zilizokuwa dukani zikidaiwa kuibiwa.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa mtaa wa Majengo Mapya, Bwana. Philimon Chikala, ameeleza kupokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa wananchi na kufika eneo la tukio kwa ajili ya hatua za awali.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa jeshi la polisi limeanza uchunguzi wa kina ambapo wanamshikilia mtuhumiwa mmoja kwa mahojiano.
Aidha Kamanda Magomi amewahimiza wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu na kuimarisha usalama katika mkoa huo.