Watu tisa akiwamo dereva wa basi la abiria la Kampuni ya Abuu Trans, wamefariki dunia huku wengine 16 wakijeruhiwa baada ya basi linalofanya safari zake kati ya Dodoma na Kondoa, kupata ajali katika eneo la Kambi ya Nyasa wilayani Chemba mkoani Dodoma, likitokea Kondoa kwenda Dodoma Mjini.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gallus Hyera amesema ajali hiyo ilitokea saa 12:40 alfajiri ya kuamkia leo Alhamisi Septemba 18, 2025 na chanzo chake ni uzembe wa dereva wa lori, aliyepoteza mwelekeo na kuingia upande wa basi na kusababisha magari hayo kugongana uso kwa uso.
Katika ajali hiyo watu watano wamefariki dunia papo hapo na wengine wanne walifariki dunia wakati wanapelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kupatiwa matibabu.
Amesema miongoni mwa waliopoteza maisha ni wanafunzi wanne aliowataja kuwa ni Carolyne Joachim (13), Rukia Ally (14), Bashir Hashim (13) na Nasra Mohamed (18).

Aidha, ametoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazotokana na uzembe.
Kamanda huyo amesema dereva wa lori ni miongoni mwa majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu na baada ya uchunguzi kukamilika, atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Ernest Ibenzi amesema walipokea taarifa za ajali saa nne asubuhi na wamepokea majeruhi tisa na majeruhi hao wamepata majeraha mbalimbali mwilini ikiwemo mikononi, miguuni na kichwani, hata hivyo hali zao zinaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu ya awali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ametoa wito kwa madereva kuhakikisha wanapumzika wanapohisi uchovu au usingizi ili kuepusha madhara.
Amesema ajali hiyo imetokea katika eneo lenye barabara nyoofu, jambo linaloashiria uzembe wa dereva.