Msanii wa muziki wa Tanzania, Barnaba Classic, amesema amepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 100 baada ya moto kuteketeza studio zake za High Table Sound Entertainment Company Limited zilizopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Juni Mosi, 2026.
Barnaba amesema moto huo ulianza majira ya saa 2:30 usiku, muda mfupi baada ya kurejea kutoka kwenye shoo ya Malkia wa Nguvu iliyofanyika Arusha, baada ya kufika Dar es Salaam, alipitia studio hizo kusalimia kabla ya kuelekea nyumbani, ambapo dakika chache baadaye alipigiwa simu na kupewa taarifa za kuzuka kwa moto.
Akizungumzia tukio hilo, Barnaba amesema moto huo uliendelea kuwaka hadi majira ya saa 4:40 usiku na kwamba chanzo chake kinadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme. Aidha, amesema walipofika eneo la tukio moto ulikuwa tayari umeenea kwa kiwango kikubwa na hawakufanikiwa kuokoa mali yoyote.
Msanii huyo amesema studio hizo zilikuwa zimefanyiwa ukarabati mkubwa wiki mbili zilizopita kwa gharama kubwa, jambo ambalo limeongeza maumivu kutokana na hasara iliyopatikana. Ameeleza kuwa kituo hicho kilikuwa tegemeo la kazi zake za muziki pamoja na vijana wengi waliokuwa wakikinufaika.
Licha ya kupoteza mali na vifaa vyote vilivyokuwemo ndani ya studio hizo, Barnaba amesema anamshukuru Mungu kwa kila jambo na kwamba yupo tayari kuanza upya, akiamini kuwa changamoto hiyo ni sehemu ya mafunzo katika maisha na safari yake ya muziki.
