
Baraza la Maaskofu wa Kitaifa wa Congo (CENCO) limelaani hukumu ya kifo iliyotolewa kwa Rais wa zamani wa taifa hilo Joseph Kabila na Mahakama Kuu ya Kijeshi ya Kinshasa.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CENCO; Monsinyo Donatien Nshole jana Jumatatu, imesainiwa na Rais wa CENCO Askofu Mkuu Fulgence Muteba.
Maaskofu hao wamedai kwamba mantiki ya kuadhibu ya hukumu ya kifo inashindwa kukuza amani au mshikamano wa kitaifa na kuelezea imani hiyo kuwa haipatani na maadili ya Injili.
Aidha wanasisitiza mazungumzo jumuishi ili kushughulikia mizozo ya DRC, wakisema, “mazungumzo jumuishi yanasalia kuwa njia bora ya kushughulikia vyanzo vya migogoro hiyo na kurejesha umoja na amani.
Kabila alihukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani kwa uhalifu wa kivita na uhaini Septemba 30, 2025.
Mashtaka hayo yanahusu shutuma kwamba Kabila amekuwa akiunga mkono kundi la M23, kundi la waasi ambalo limesababisha uharibifu katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.